2 Chronicles 14

Asa Atawala

1 aNaye Abiya akalala na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme baada yake. Katika siku zake, nchi ikawa na amani kwa miaka kumi.

2Asa akatenda yaliyo mema na haki machoni pa Bwana Mwenyezi Mungu wake. 3 bAkaziondoa madhabahu za kigeni na mahali pa juu pa kuabudia miungu, akayavunja yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Maashera. 4Akawaamuru Yuda kumtafuta Bwana, Mungu wa baba zao na kutii sheria zake na amri zake. 5 cAkaondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu na madhabahu za kufukizia uvumba kwenye kila mji katika Yuda, nao ufalme ulikuwa na amani katika utawala wake. 6 dAkajenga miji yenye ngome katika Yuda, wakati nchi ikiwa na amani. Hakuna mtu yeyote aliyepigana vita naye katika miaka hiyo, kwa kuwa Bwana alimstarehesha.

7Mfalme akawaambia Yuda, “Tuijenge hii miji na tuizungushie kuta, pamoja na minara, malango na makomeo. Nchi bado ni yetu, kwa sababu tumemtafuta Bwana Mwenyezi Mungu wetu, tulimtafuta naye ametupa raha kila upande.” Hivyo wakajenga na wakafanikiwa.

8Asa alikuwa na jeshi la watu 300,000 kutoka Yuda, wenye ngao kubwa na mikuki na jeshi la watu 280,000 kutoka Benyamini, wenye ngao ndogo na pinde. Watu hawa wote walikuwa wapiganaji mashujaa.

9 eZera Mkushi akatoka kupigana dhidi yao akiwa na jeshi la watu maelfu ya maelfu na magari ya vita 300, nao wakaja mpaka Maresha. 10Asa akatoka kumkabili, nao wakapanga vita katika Bonde la Sefatha karibu na Maresha.

11 fKisha Asa akamlilia Bwana Mwenyezi Mungu wake na kusema, “Ee Bwana, hakuna yeyote aliye kama wewe wa kuwasaidia wasio na nguvu dhidi ya wenye nguvu. Utusaidie, Ee Bwana, wewe ndiwe Mungu wetu, kwa kuwa tunakutumainia wewe, nasi kwa jina lako tumekuja dhidi ya jeshi hili kubwa. Ee Bwana, wewe ndiwe Mungu wetu, usiwaache wanadamu wakushinde wewe.”

12 g Bwana akawapiga Wakushi mbele ya Asa na Yuda. Wakushi wakakimbia, 13 hnaye Asa na jeshi lake wakawafuatia mpaka Gerari. Idadi kubwa ya Wakushi ilianguka hata wasiweze kuinuka tena, wakapondapondwa mbele za Bwana na majeshi yake. 14 iWatu wa Yuda wakachukua nyara nyingi sana, wakaangamiza vijiji vyote vinavyoizunguka Gerari, kwa kuwa hofu ya Bwana ilikuwa imewaangukia. Wakateka nyara vijiji hivi vyote, kwani kulikuwepo nyara nyingi huko. 15Pia wakashambulia kambi za wachunga makundi ya wanyama wakachukua na kuyaswaga makundi ya kondoo, mbuzi na ngamia. Kisha wakarudi Yerusalemu.
Copyright information for SwhKC